Jumatano, 8 Mei 2013

MZEE MWINYI NA SALIM WANUSURU KUUZWA KWA JENGO LA SKAUTI

 Mzee Ali Hassan Mwinyi Mdhamini wa Skauti Tanznia (Rais Mstaafu wa Tanzania)

Wadhamini wa Chama cha Skauti Tanzania Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi na Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim (pia alikuwa Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika-OAU)  wameingilia kati katika hatua za kunusuru jengo la Skauti Makao Makuu  lililopo Upanga jijini Dar Es Salaam lisiuzwe kwa mnada  na Kampuni ya Madalali ya Flamingo kufuatia utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya Kazi.

Katika mahojiano na 'Chombo cha habari cha Skauti Dar Es Salaam' Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito Brigedia Jenerali Mstaafu Gerald Mkude alibainisha kuwa, tarehe 28 Aprili, 2013 alipigiwa simu na msaadizi wa Mzee Mwinyi na kumtaka kuwepo na kikao cha dharura kati ya wadhamini wa chama pamoja na viongozi wa kamati zote mbili (kamati ya mpito ikiongozwa na Ndugu Mkude na kamati tendaji ikiongozwa na Balozi Kuhanga). "Nilitoa taarifa kwa wenzangu kwa kuwepo na kikao cha dharura na wadhamini wa chama na tarehe 29 Aprili, 2013 tulikaa kikao" alisema ndugu Mkude.
Ndugu Mkude alieleza kuwa katika kikao hicho wadhamini wa chama walihoji sababu zilizopelekea kukamatwa kwa jengo na kutaka kuuzwa kwa mnada ndani ya siku 14. "Niliwaelezea sababu hizo na kuwapa taarifa tulizozichukua kwa muda huo" alisema ndugu Mkude.
Pia katika kikao hicho wadhamini wa chama Rais Mstaafu Mzee Mwinyi na Waziri Mkuu Mstaafu Dkt Salim Ahmed Salim walizitaka kamati zote mbili kufuata taratibu za kisheria haraka kwa ajili ya zuio la mahakama kupisha hatua zaidi ya kunusuru jengo hilo.

Wakili wa kujitegemea kutoka katika Kampuni ya Mawakili ya APEX ATTORNEYS walipendekezwa katika mchakato wa kutetea kuuzwa kwa jengo la Skauti, tarehe 5 Mei, 2013 wakili wa Apex Attorneys na Mwenyekiti wa  Kamati ya Mpito Brigedia Jenerali Mstaafu Gerald Mkude walipitia mapendekezo na sababu za zuio (Stop Order) la kupinga hukumu ya mahakama ya kazi kukamata na kutaka kuuzwa kwa mnada jengo la Skauti Upanga Dar Es Salaam.
"Tarehe 6 Mei, 2013 wakili wetu alinitaarifu kuwa Mahakama Kuu imekubali ombi letu na hukumu inachapishwa" alisema Ndugu Mkude.
7 Mei, 2013 Msajili wa Mahakama Kuu aliridhia sababu za kutouzwa kwa jengo na kutaka pande zote mbili (mdai na mdaiwa) kukutana na kuafikiana madai halali ya malipo ya mdai Bi. Agnes George.

MAHESABU YATOFAUTIANA

Katika hali isiyo ya kawaida, baada ya kupitia makalablasha mawakili wanaokiwakilisha Chama cha Skauti Tanzania wabaini kiwango cha madai na hoja ya msingi anayodai Bi. Agnes George yanatofauti kubwa, yanakadiliwa kufikia Milioni tano Shilingi za Kitanzania tofauti na hoja yake ya msingi ya madai ya Tsh 111,510,384.60.

Brigedia Jenerali Mstaafu Ndugu Gerald Mkude Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito.
Ndugu Mkude alieleza kuwa, kesi itasikilizwa tarehe 23 Mei, 2013 Mahakama Kuu ambapo upande wa mdai Bi. Agnes George na mdaiwa Skauti Tanzania watawasilisha maoni yao kuhusu uhalali wa madeni yao kwani upande wa mdai unahoja ya kudai 111,510,384.60 na mdaiwa ukiwa na hoja ya kudaiwa  kiasi kinachokadiriwa kutozidi Milioni Tano fedha za Kitanzania.
"Suala la mnada limesitishwa, ninawashukuru wadhamini wa chama kwa kutuongoza vyema, nawashukuru pia kamati zote mbili na wanachama wote wa Skauti kwa mchango wao wa hali na mali, utulivu, maombi na dua zao katika hali hii" alisema Ndugu Mkude na kuahidi kutoa ushirikiano na taarifa kwa wakati katika kipindi hichi.

HATI YA PINGAMIZI