Jumamosi, 27 Aprili 2013

Skauti Tanzania Yauzwa..!!?

Katika jambo kubwa la kuwagubika giza na mshangao usio na mfano, Skauti wa Tanzania walipopata habari za Jengo na eneo la Makao Makuu ya chama hicho litapigwa mnada ndani ya siku 14 kuanzia tarehe 24/04/2013 endapo chama kitashindwa kulipa fedha za Kitanzania zaidi ya Milioni Mia Moja.

Bango lililobandikwa katika ofisi ya Makao Makuu ya Skauti Tanzania, linaloijulisha Umma kuwa jengo hilo limekamatwa na Mahakama Kuu ya Kazi
Tarehe 24 mwezi Aprili mwaka 2013 majira ya asubuhi baadhi ya maofisa kutoka Kampuni ya Mnada ya Flamingo walifika ofisi za Makao Makuu ya Skauti Tanzania zilizopo Dar Es Salaam, wilaya ya Ilala eneo la Upanga, maofisa hao wakiwa na Hati ya kukamata nyumba kiwanja namba 1078 na Lo 120652, inayoonyesha madai ya jumla ya Tzs 114,855,686.13 na kumtaka katibu mhuktasi wa chama hicho kusaini mapokeo ya hati hiyo na kukubaliana malipo ya madai hayo yalipwe ndani ya siku kumi na nne tokea siku hiyo.  Katibu mhuktasi huyo alikataa kusaini na kuchukua jukumu la kumpigia simu ya mkononi Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito ndugu G. Mkude (Brigedia Jenerali Mstaafu) ambaye alimtaka katibu mhuktasi huyo kutopokea ama kusaini mpaka yeye afike ofisini. Badala yake maofisa hao wa kampuni ya Mnada ya Flamingo walibandika  bango (Hati) hiyo katika eneo la kubandika matangazo la chama hicho (kama linavyosomeka hapo juu)

Skauti ni chama cha watoto na vijana wakiongozwa na watu wazima, leo hii  wasimamizi wameshindwa wajibu wao, na kuacha mali zao zikitingishwa kwa njinsi watakavyo wao.

SKAUTI WAKUTANA

Tarehe 24/04/2013 baada ya kubandikwa kwa bango la hati ya kukamatwa kwa jengo la chama chao, baadhi ya Skauti wa Mkoa wa Dar Es Salaam walikutana kwa dharura katika viwanja vya makao makuu ya chama chao kwa kutaka kujua ukweli wa jambo hilo.

"Haya yote yanatokana na tamaa zilizoambukizwa na gonjwa linalosababishwa na uloo wa chakula cha ufisidi" alisikika akisema mpita njia ambaye hakufahamika jina.

CHANZO

Katika miaka ya nyuma aliyewai kuwa mfanyakazi kama katibu mhuktasi Bi. Agnes George alikuwa na madai yanayokadiliwa kufikia milioni tano kama malipo ya kiinua mgongo na usafiri. Alifungua kesi ya madai iliyopelekea kuuzwa kwa mnada gari aina ya SUZUKI - Vitara mali ya chama hicho utekelezaji wa hukumu ya Mahakama.

TATIZO

Baadhi ya Skauti wamefunguka na kusema 'tatizo kubwa linalokisumbua chama chetu kwa sasa ni kutokuwa na uongozi' Chama chetu kwa sasa kinaendeshwa na Kamati ya Mpito iliyoteuliwa na Rais wa chama ambaye ni Waziri wa Elimu (Mhe. Dr Shukuru Kawambwa).

Akiongea na baadhi ya Skauti waliokuwa katika eneo la kiwanja cha Skauti makao makuu siku hiyo ya tukio ya kubandikwa kwa hati ya kukamata nyumba (jengo la Skauti) Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito ndugu G. Mkude (Brigedia Jenerali Mstaafu) alisema "Kamati hii ya mpito imemaliza muda wake tangu tarehe 6/03/2013, niliandika barua ya kuomba muongozo kwa rais wa chama na nakala ya barua hiyo kumpelekea Mwenyekiti wa kamati tendaji" aliendelea kubainisha "Tarehe 5/04/2013 rais wa chama akatuongezea muda wa miezi 3 mbele zaidi" mwisho wa kunukuu.

Ndugu Mkude aliwaeleza Skauti hao kuwa ameitisha kikao cha dharura siku ya jumatatu tarehe 29/04/2013, kikao hicho ni cha kamati zote mbili, kamati ya mpito ikiongozwa na ndugu Mkude na kamati tendaji ikiongozwa na Balozi Kuhanga. Kikao hicho kitajadili suala la hati ya kukamatwa kwa jengo la chama chetu.

MKUU WA WILAYA YA ILALA

Kipindi cha takribani wiki moja kabla ya tukio hilo, baadhi ya Skauti walikuwa wanatumiana ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kuhusiana na uongozi wa Skauti na Uskauti.

Baadhi ya watu wasiopenda mafanikio ya Skauti Tanzania walitumia nafasi hii kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi uliohamasisha Skauti kuandamana kupinga uzembe uliofanywa na uongozi kupelekea kukamatwa  kwa jengo hilo. Ujumbe huo ulifika kwa baadhi ya Viongozi wa Serikali na taasisi zake za kiusalama.

Taarifa hiyo ilimlazimu Mkuu wa Wilaya ya Ilala kumuagiza afisa tarafa wa tarafa ya Kariakoo ndugu Muyanjo akiambatana na Polisi tarafa wa tarafa hiyo Insp. Ibrahimu kwenda makao makuu ya chama chetu kujua ukweli wa jambo hilo. Viongozi hao walikutana na Mwenyekiti wa kamati ya mpito  ndugu G. Mkude (Brigedia Jenerali Mstaafu) pamoja na Kamishina wa Skauti wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Ndugu Abubakari Mtitu.

"Sisi ni taasisi yenye nidhamu, hekima na heshima tunashirikiana kwa pamoja na Serikali na baadhi ya taasisi zake nyingi kwa shughuli zetu za kila siku, hatufikirii kuandamana wala hatuna nia hiyo, tupo hapa kutaka kujua au kusikia kutoka kwa viongozi wetu" alisema mmoja wa Skauti, akiwaambia Skauti wenzake pamoja na Afisa tarafa na Polisi tarafa wa Kariakoo katika kikao hicho kisicho rasmi