Jumamosi, 30 Desemba 2017

Ijumaa, 24 Machi 2017

TSA yawawezesha Waelekezaji wa 'U-Report'

Balo Emmanuel, Meneja wa Mradi wa U-Report kutoka UNICEF akielezea jambo katika Warsha ya Wawezeshaji wa mradi huo katika Ukumbi wa hotel ya Ndekha jijini Dar es Salaam, tarehe 23/03/2017 (Picha na Sassi)


Habari na Crispin Majiya (PR Lab), Dar es Salaam


Chama cha Skauti Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kuhudumia Watoto (UNICEF) kimefanya Warsha ya Siku Mbili Jijini Dar es Salaam yenye lengo la kuwawezesha Makamishna wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wawakilishi wa Majukwaa ya Vijana kutoka Mikoa na Wilaya zao.

Warsha hii ni Awamu ya kwanza ya Mradi wa U-Report unaotekelezwa na Chama cha Skauti Tanzania, chini ya Udhamini wa UNICEF, ambapo katika Awamu hii Washiriki wanawezeshwa kuwa Waelekezi ambao watarudi Mikoani kwao kufundisha Vijana ambapo kila Kamishna wa Mkoa atawezeshwa kufanya kambi yenye Washiriki Vijana wasiopungua Sitini. hii itakuwa ni Awamu ya Pili ya Mradi wa U-Report.
Bi. Easter Peter Riwa Mkurugenzi Msaidizi Kazi na Maendeleo ya Vijana na Watu Walemavu Ofisi ya Waziri Mkuu akifungua Warsha hiyo.
U-Report ni programu maalum kwa ajili ya kutoa taarifa kwa matukio mbalimbali yanayotokea kwenye jamii zetu kama vile unyanyasaji wa watoto / kijinsia, matukio ya uhalifu, ajira za utotoni na ukatili dhidi ya watoto.

Aidha, imetolewa rai ya kujiunga kwa kutumia sms yenye neno 'SAJILI' kwenda namba '15070' na sms zote ni Bure (bila ya kutozwa gharama yoyote).

Huduma hii inapatikana kwa watumiaji wa mitandao ya simu ya kiganjani ya Tigo, Vodacom, Airtel na Zantel. Aidha mradi huo unatarajia kujiunga na mitandao mingine ya simu ya kiganjani ya Halotel pamoja na TTCL.

Aidha pamoja na uwezeshaji huu, washiriki walipata mafunzo kuhusu baadhi ya Sera za Chama cha skauti Tanzania jinsi zinavyoendana na programu hii ya U-Report. Sera hizo ni Sera ya Ulinzi wa Mtoto, Sera ya Programu za Vijana pamoja na Programu yenyewe. Pia walijifunza kuhusu Jinsi U-Report inavyoweza kutumika katika Ujumbe wa Amani (MoP) na Majadiliano, na kukabiliana na Maafa.



Baadhi ya washiriki wa Warsha wakisikiliza kwa makini



Mhariri na Picha: Sassi
Habari kwa Msaada wa TSA-PR Lab
(c)Tanzania Scouts Association - PR Lab 2017

Alhamisi, 23 Februari 2017

Rais Mstaafu Mzee Mwinyi Aongoza Matembezi ya Skauti Dar

2-14
Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza, akizungumza jambo baada ya kuhitimisha matembezi (Tarehe 18/02/2017)


RAIS mstaafu ambaye pia ni Mdhamini wa Skauti Tanzania, Mzee  Ali Hassan Mwinyi,  leo (tarehe 18/02/2017) ameongoza matembezi ya hisani (Charity Walk) kwa ajili ya kuchangisha fedha  za kufanikisha shughuli za Chama cha Skauti Tanzania  kutoka kwa wadau na marafiki wa skauti kuelekea maadhimisho ya siku ya Skauti Afrika yanayotarajiwa kufanyika Machi 8 hadi 11 na Miaka 100 ya Skauti Tanzania (1917 - 2017) matukio yote mawili yanategemea kufanyika mwaka huu jijini Arusha.


Matembezi hayo ya hisani yameanzia katika kiwanja cha Skauti kilichopo Upanga jijini Dar es Salaam na kuishia katika bwalo la Maofisa wa Polisi (Police officers Mess) la Oysterbay kuanzia saa 12 asubuhi na kufikia tamati majira ya saa nne asubuhi.

1-15
Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi (wa pili kushoto) alipofika katika viwanja vya Bwalo la Polisi, Oyster Bay jijini Dar, wakati alipohitimisha matembezi ya hisani. Kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako aliyeungana naye.


Aidha, Rais Mstaafu ALI HASSAN MWINYI, amezindua mfuko wa kuchangia maandalizi ya mkutano wa Skauti wa Afrika, uanaotarajiwa kufanyika Arusha, Machi mwaka huu ambapo ameonyesha kufadhaishwa na baadhi ya wazazi wanaoshindwa kuwalea watoto wao katika roho na kweli hivyo kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa maadili na kihalifu ikiwemo matumizi ya vileo na dawa za kulevya.
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa zaidi ya watu 5,000 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya bara hilo wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano wa mwaka wa maskauti kuanzia Mach 8 mpaka 11 mwaka huu Mkoani Arusha, ikiwa ni maadhimisho ya kila mwaka ya siku ya skauti Afrika yanayokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 1OO ya skauti Tanzania.
Mzee Mwinyi, ambaye ni Mwenyekiti wa baraza la wadhamini wa skauti Tanzania,mwenye umri wa miaka 93 sasa, akiwa bado ni mkakamavu na mwenye siha njema, alitembea kilometa 6.5 kutoka Makao makuu ya skauti Upanga mpaka viwanja vya bwalo la maafisa Polisi Ostabei, katika matembezi ya hisani kuchangia maandalizi ya mkutano huo unaotarajiwa kugharimu shilingi milioni 800.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na mafunzo ya Ufundi, Profesa JOYCE NDALICHAKO, ambaye kwa mujibu wa katiba ya skauti ni Rais wa skauti kutokana na madaraka yake, amewasihi wazazi kuwapeleka watoto wao skauti wakajifunze maarifa, stadi za maisha na uzalendo, badala ya kuwaacha kama mifugo isiyo na mchungaji na katika hatua nyingine, amewaonya walimu wote amabo shule zao zitabainika kuwa vijiwe vya wanafunzi kujifunzia mambo yasiyofaa, serikali haitawavumilia.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa matembezi hayo, Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza,  alisema kuwa chama hicho kinatarajiwa kusherehekea Siku ya Skauti Afrika na kuadhimisha miaka 100 tangu Skauti kuingia Tanzania Bara (Tanganyika).  Chama hicho hapa nchini kilianza mwaka 1917 na mwaka huu wa 2017 kinatimiza miaka 100.
Uchangishaji mwingine wa fedha kwa njia ya chakula (Dinner Gala Fund Raising) unategemea kufanyika Februari 24  katika Hoteli ya Serena ya ijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake kamishna Mkuu wa Skauti Abdulkarimu Shah amesema bado wanaendelea kuwahamasisha vijana kujiunga katika chama hicho ili kuwa waadilifu, wajasiri, wabunifu na wenye maarifa ili kufanikiwa na kuepukana na magonjwa yanayoepukika ikiwemo Ukimwi.
Maadhimisho hayo yatafanyika juni 24 hadi julai mosi mwaka huu mjini Arusha, yenye kauli mbiu inayosema “kuwajenga wazalendo na kufanya kazi kwa bidii kwa maendeleo ya nchi”.







Jumapili, 12 Februari 2017

Matembezi ya Hisani (Scouts Charity Walk 2017)



Chama cha Skauti Tanzania kuelekea kusherehekea Siku ya Skauti Afrika na kuazimisha miaka 100 tangu Skauti kuingia Tanzania Bara (Tanganyika).

Skauti ulianza mwaka 1917 na mwaka huu wa 2017 Skauti inatimiza miaka mia moja, Kwa kutaka kufanikisha zaidi Chama cha Skauti Tanzania kimeandaa matembezi ya hisani (Charity Walk) ili kuweza kupata fedha kutoka kwa wadau na marafiki wa Skauti.

Pamoja na matembezi hayo ya hisani yenye lengo la kukusanya pesa za matukio hayo makubwa ya Kitaifa, Chama cha Skauti Tanzania (TSA) pia imeandaa chakula cha kuchangisha fedha kwa mazumuni hayo hayo katika kusaidia watoto na vijana kufanikisha dhima yao.

Matembizi ya hisani yatafanyika siku ya Jumamosi tarehe 18 mwezi wa Februari 2017 kuanzia katika kiwanja cha Skauti kilichopo Upanga barabara ya Malik na kuishia katika bwalo la Polisi la Oysterbay kuanzia saa 12 asubuhi.

Matembezi hayo ya hisani yataongozwa na Mdhaminiwa Skauti Tanzania Mh. A. H. Mwinyi (Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania).
Mheshimiwa Mwinyi amekuwa akiongoza matembezi mengi ya hisani hapa Tanzania, hii ni kwa kuwa ni mtu ambaye anapenda sana kufanya mazoezi.

Uchangishaji fedha kwa njia ya chakula (Dinner Gala Fundraising) inategemea kufanyika tarehe 24 Februari 2017 katika hioteli ya Serena iliyopo jijini Dar es Salaam.

Matembezi hayo ambayo mtandao mkubwa na mpana wa kijamii wa Skauti Scouts Chat Forum (SCF360) imeyapa jina la kuamasisha la #NiMatembeziYe2 katika kuamasisha katika mitandao ya kijamii na kuwesambaza picha mbalimbali za uamasishaji.



Siku ya Skauti Afrika inatarajiwa kufanyika tarehe 8 hadi 11 Machi, 2017 Arusha katika kitongoji cha Kisongo.

Alikadhalika Miaka 100 ya Skauti Tanzania pia yatafanyika Kisongo, Arusha kuanzia tarehe 24 Jun1 hadi 1 julai 2017 na matukio yote mawili yanatarajiwa kuhudhuriwa na Skauti kutoka ndani na nje ya Tanzania (Afrika na nje ya bara la Afrika)

Kwa Usajili na habari zaidi waweza kutembelea kurasa hizi:-