- ATOA TAARIFA KWA WANACHAMA WA CHAMA CHA SKAUTI TANZANIA
- KUFANYIKA KWA KAMBI YA TAIFA YA VETERANI
Kamishna Mkuu wa Skauti Tanzania (pia Mbunge wa Mafia na Mwenyekiti wa Skauti Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) Mhe. Abdulkarim Esmail Hassan Shah, akizungumza kabla ya kutoa taarifa yake, alizungumzia kero ambazo dhahiri zinaonyesha kutokuwa na heshima, nidhamu na kusahau kanuni na ahadi ya Skauti kwa baadhi ya Skauti wachache. Kamishna Mkuu Mhe. Shah alikumbusha kuwa ni wajibu wa kila Skauti kufuata taratibu, ahadi, kanuni na katiba ya chama cha Skauti.
Kamishna Mkuu alisema, "Kero yangu ipo kwa baadhi ya Skauti kusambaza ujumbe mfupi maandishi wa simu ya kiganjani, wenye maneno yasiyofaa" Mhe. Shah aliendelea kusema, "ndugu zangu Skauti, tusubiri tujichafue wenyewe sio kuanza kutuchafua" Kamishna Mkuu alisisitiza kwamba hatua kali na za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya Skauti yeyote hasiyefuata taratibu za Skauti.
Nae Naibu Kamishna Mkuu wa Skauti Tanzania ndugu Rashid Kassim Mchatta, katika salaamu zake za kushukuru kwa kuteuliwa na kuapishwa kwa nafasi hiyo alisema, "Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua hii, sina mengi ya kusema zaidi ya kuahidi kushirikiana na Skauti wote, lakini siko tayari kushirikiana na Skauti ambaye hataki kutimiza wajibu wake, kufuata kanuni, ahadi na katiba ya chama chetu"
Katika taarifa yake kwa wanachama wa chama cha Skauti Tanzania, Kamishna Mkuu wa Skauti Mhe. Shah alisema;
"1. Kufuatia Mkutano Mkuu Maalum wa Baraza Kuu la Skauti uliofanyika tarehe 05 Januari 2013, majina matatu ya wagombea wa nafasi ya Skauti Mkuu yaliwasilishwa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mlezi wa Chama cha Skauti Tanzania.
Mgeni wa heshima ambaye ndiye mdhamini wa Chama cha Skauti Tanzania Mzee Ally Hassan Mwinyi (Rais mstaafu) [katikati] akijiandaa kutoa hutuba katika Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu ulifanyika tarehe 05 Januari 2013 katika ukumbi wa Don Bosco Upanga Dar Es Salaam. Kulia ni Rais wa Chama cha Skaut Mh. Shukuru Kawambwa (Waziri wa Elimu) na kushoto ni Prof. W. Salungi (Makamo Mwenyekiti) wa mkutano mkuu. |
2. Kwa madaraka aliyonayo katika katiba ya Chama cha Skuti Tanzania, Mlezi wa Chama alimteua na kumuapisha Mheshimiwa Mwantumu Bakari Mahiza kuwa Skauti Mkuu (Chief Scout). Hii ilikuwa tarehe 24 Juni, 2013.
Mhe. Abdulkarim Shah akiapa kuwa Kamishna Mkuu wa Skauti Tanzania, tarehe Julai 12, 2013 |
3. Baada ya uteuzi wa Skauti Mkuu, Kamati Tendaji ya Chama ilifanya Mkutano Maalum wa uchaguzi wa Kamishna Mkuu (Chief Commissioner) wa Chama. Kwa kuzingatia katiba ya Chama, Kamati iliwasilisha majina ya wagombea kwa Skauti Mkuu kwa ajili ya uteuzi. Skauti Mkuu ameniteua na kuniapisha mimi Abdulkarim Esmail Hassan Shah kuwa Kamishna Mkuu. Hii ilikuwa tarehe 12 Julai, 2013.
Naibu Kamishna Mkuu, Ndugu Mchatta akiapa kushika nyadhifa hiyo |
4. Katika hatua ya kuendelea kukamilisha safu ya Uongozi, leo (tarehe 19 julai, 2013) nimemuapisha Ndugu Rashid Kassim Mchatta kuwa Naibu Kamishna Mkuu (Deputy Chief Commissioner) wa Chama cha Skauti Tanzania. Aidha uteuzi wa Makamishna Wakuu Wasaidizi (Assistant Chief Commissioner) utafanyika hivi punde. Hawa kwa pamoja watakamilisha safu ya uongozi katika Kamati ya uendeshaji.
5. Ili kuimarisha uongozi wa Chama Mikoani na Wilayani nitatoa waraka wa kutengua madaraka kwa waliokuwa Makamishna na Manaibu wao Mikoani na Wilayani. Kikatiba nafuta waranti za Makamishna wote na zinatakiwa kurejeshwa Makao Makuu ya Chama ifikapo tarehe 15 Agosti, 2013. Uteuzi wa Makamishna wapya utafanywa katika siku chache zijazo. Katika kipindi hichi cha mpito, Makamishna wa Mikoa na Wilaya wataendesha ofisi hadi hapo uteuzi mpya utakapofanywa.
6. Natoa wito wa ushirikiano kutoka kwa viongozi na wanachama wote ili zoezi hili la kupata safu nyingine ya uongozi likamilike kwa kuzingatia kauli mbiu ya "UONGOZI IMARA CHAMA IMARA"
Pamoja na taarifa hiyo kwa wanachama wote wa Chama cha Skauti Tanzania, Kamishna Mkuu Mhe Shah alipongeza na kutoa hongera kwa kazi nyingi za kujitolea zilizofanywa na zinazoendelea kufanyika na Skauti Tanzania, vilevile Mhe. Shah aligusia kufanyika kwa kambi ya Taifa ya Skauti wa zamani (Veterani) kuanzia tarehe 16 hadi 18 Agosti, 2013.
Kamishna Mkuu wa Skauti alimpa majukumu ya uandaaji wa kambi hiyo na kumwagiza Kaimu Kamishna wa Skauti Mkoa wa Dar Es Salaam ndugu Abubakar Mtitu, kuunda kikosi kazi (Task Force) cha kushirikiana kukamilisha kambi hiyo, kwa kufuata na kuzingatia taratibu na maamuzi ya vikao kabla ya kambi hiyo.
Tufuate Twitter: @DarScout http://www.twitter.com/DarScout
Facebook: Dar Es Salaam Scout https://www.facebook.com/daressalaamlocalscoutassociation
Scout Face: http://www.scoutface.org/Dar Es Salaam Scout