Ijumaa, 12 Juni 2015

MZEE NGUNGA AFARIKI DUNIA

PENGO LAKE HALITAZIBIKA

NI VETERANI SKAUTI ALIYEKABIDHIWA SKAUTI NA WAKOLONI


Chama cha Skauti Tanzania (TSA) kimepatwa na pigo lingine la kuondokewa na kipenzi chake aliyeanza Skauti tangu enzi ya Ukoloni.

Marehemu Ndugu Isdor Stanslaus Ngunga alizaliwa tarehe 12 Januari 1928 katika kijiji cha Mwenge Mshindo, Wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma na alijiunga katika Chama cha Skauti Tanzania Mkoa wa Ruvuma mwaka 1940 akiwa ni mwanafunzi katika shule ya Mtakatifu Benedict (Father Benedict Middle School) iliyopo Peramiho Mkoani Ruvuma.

Marehemu Mzee Isdor Stanslaus Ngunga, enzi ya uhai wake akiwa nyumbani kwake alipotembelewa na waandishi wa Dar Scout Media kwa mahojiano.

Marehemu alipenda sana mafunzo ya Skauti na kuendelea nayo hadi alipojiunga na Elimu ya juu katika Chuo hicho hicho cha Mtakatifu Benedict, Peramiho.

Marehemu Mzee Ngunga alipata mafunzo mbalimbali ya Skauti ndani na nje ya nchi. 

  • Alipata Mafunzo ya Mwanzo ya Uongozi (PTC) mwaka 1950
  • Mafunzo ya Skauti (Wood Badge - WB) mwaka 1955.

UONGOZI

Amewai kushika nafasi mbali mbali za uongozi ambapo mwaka 1955 aliteuliwa kuwa Kiongozi wa Skauti, yaani "Scout Master" wa kundi la Skauti la Litembo mjini Songea.
  • Mwaka 1960 aliteuliwa kuwa Kiongozi wa Skauti wa Wilaya (District Scout Master) katika Wilaya ya Songea.
  • Mwaka 1961 aliteuliwa kuwa "Field Commissioner" Makao Makuu ya Chama cha Skauti Tanzania.
  • Mwaka 1979 aliteuliwa kuwa Kamishna Mkuu Msaidizi wa Mafunzo Tanzania.
  • Mwaka 1994 aliteuliwa kuwa Kamishna Mkuu Msaidizi Mambo ya Nje.
  • Mwaka 1992 aliteuliwa kuwa Naibu Kamishna Mkuu Tanzania.
  • Mwaka 1998 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mafunzo katika Chama cha Skauti Tanzania.
  • Mwaka 2008 hadi mauti yake aliteuliwa kuwa Mshauri wa Chama cha Skauti Tanzania.

Skauti wakiwa wamebeba sanduku la mwili wa Marehemu Mzee Ngunga kutoka nyumbani kwake Kijitonyama barabara ya Akachube kuelekea Kanisani kwa maombi, tarehe 17 Juni 2015 siku ya Jumatano.
Marehemu Ndugu Isidori Ngunga katika shughuli zake za kazi kama Mwalimu katika Chuo cha Ualimu Peramiho na baadae Nangosho Mbambabay, Seminary ya Kigonsera, Litembo na Mtyangimbole huko Ruvuma aliendelea na shughuli za Skauti, shughuli ambazo alizipenda na pia alifurahi kuona wanafunzi wake wengi wakijiunga na Chama cha Skauti.

KUTOKA WIZARANI HADI SKAUTI

Akiwa ni Mtumishi wa Wizara ya Elimu mara baada ya Nchi yetu kupata Uhuru mwaka 1961, Marehemu Ndugu Isidori Stanslaus Ngunga aliazimwa kutoka Wizara ya Elimu na kufanya kazi kama Field Commissioner katika Chama cha Skauti Tanzania Makao Makuu, kazi ambazo zilimlazimu kusafiri ndani na nje ya nchi, alifanya shughuli za Skauti katika mikoa ya Shinyanga, Dar es Salaam na baadae Lagoni nchini Nigeria.

Kati ya mwaka 1975 hadi 1978 Marehemu Ndugu Isidori Ngunga aliteuliwa na Wizara ya Elimu kuwafundisha  Wakufunzi wa Umoja wa Vijana wa TANU/CCM mafunzo ya Ujasiri na Maarifa na kuwafanya wawe wakakamavu kama vijana wa Skauti.

Marehemu Isidori Ngunga (aliyevaa sare ya Skauti) enzi ya uhai wake katika picha ya pamoja na baadhi ya wajukuu na watoto wake, picha hii alipigwa Juni 14, 2014 alipotembelewa na Dar Scout Habari kwa mahojiano ya kuweka kumbukumbu za Skauti.

Mwaka 1974 hadi 1993 Marehemu Ndugu Isidori Stanslaus Ngunga katika kutimiza majukumu yake ya kikazi kama Mwalimu katika shule za Sekondari Jangwani na Mtakatifu Anthony zote za Jijini Dar Es Salaam aliendelea na Skauti kwa wakati huo akiwa ni Mshauri na Mkufunzi wa Chama cha Skauti Tanzania Makao Makuu.

Marehemu Ndugu Isidori Stanslaus Ngunga atakumbukwa daima na Uongozi wa Skauti na Ma-Skauti ndani na nje ya nchi kutokana utendaji wake mahiri na usimamizi mzuri wa Program za vijana na viongozi wa Skauti kwa ujumla.

Aidha Marehemu Ndugu Isidori Stanslaus Ngunga alishiriki kikamilifu katika shughuli ya marekebisho ya Katiba mpya ya Chama cha Skauti Tanzania, Katiba ambayo hadi hivi sasa bado ipo katika hatua za mwisho.

Baadhi ya Skauti wakiwa katika kaburi la Marehemu Mzee Ngunga wakiimba nyimbo ya Skauti baada ya mazishi ya Mzee Isdor Ngunga katik makaburi ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam, tarehe 17 Juni 2015 Siku ya Jumatano.

Baadhi ya Skauti wakiwa katika maombi katika kaburi la Marehemu Mzee Isidori Ngunga.
Kamishna Mtendaji Ndugu Eline Kitaly kwa niaba ya Skauti Mkuu na Ma-Skauti wote Tanzania akisoma wasifu wanVeterani Marehemu Isidori Stanslaus Ngunga katika makaburi ya Kinondoni Jijini Dar Es Salaam baada ya mazishi. Tarehe 14 Juni 2015, siku ya Jumatano.

Skauti wakiwasha mishumaa katika kaburi la Marehemu Ngunga


Marehemu Ndugu Isidori Stanslaus Ngunga alikuwa Mtunzi na Mwandishi wa Vijarida mbalimbali vya Mafunzo ya Skauti na kama Chama tunaahidi kuendeleza pale alipoishia.

Chama cha Skauti Tanzania tutamkumbuka daima Marehemu Veterani, Skauta, Mkufunzi na Mshauri wa Chama cha Skauti Tanzania ambaye ametutoka ghafla, pengo ambalo litachukua muda mrefu kuzibika.

Chama cha Skauti Tanzania tumempoteza Kiongozi mahiri, hodari, Shupavu na Mchapakazi, ambaye tutamkumbuka na kuenzi jina lake daima.

Sisi sote tulimpenda, lakini MUNGU amempenda zaidi.


Viongozi wa Skauti mbalimbali walikuwepo katika mazishi ya Marehemu Mzee Isidori Ngunga

Padri akiongoza misa ya kumuombea Marehemu Mzee Ngunga, Kanisani RC Mwananyamala.



Skauta Kiluswa akitoa heshima yake ya mwisho kwa Marehemu Mzee Ngunga, nyumbani kwa marehemu Kijitonyama, Jijini Dar Es Salaam.



Kamishna Mtendaji Ndugu Eline Kitaly akitoa heshima yake ya mwisho kwa Marehemu Mzee Ngunga, nyumbani kwa marehemu Kijitonyama, Jijini Dar Es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati Tendaji (TSA) Barozi Nicolaus Kuhanga (aliye vaa shati la kitenge) akifarijiana na Makamo Mwenyekiti Kamati Tendaji Mzee Mwaking'inda (aliye vaa shuti) wakati wa mazishi ya Marehemu Mzee Ngunga katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar Es Salaam. 


BURIANI Prof. Isidori Stanslaus Ngunga

12-01-1928 --- 07-06-2015














TUNAMUOMBA MWENYEZI MUNGU AIPUMZISHE ROHO YAKE MAHALI PEMA PEPONI.

AMEEN.





Habari hii kwa msaada wa Chama cha Skauti Tanzania
Kwa habari zaidi ya mahojiano ya Marehemu Ndugu Isdor Stanslaus Ngunga na Dar Scout Habari, yaliyofanyika 14 Julai 2014, picha na habari za Viongozi wa Skauti, Skauti na chimbuko pamoja sababu ya Marehemu Ngunga kuuitwa Professor wa Skauti Tanzania. Tembelea ukurasa huu tarehe 21 Juni 2015.

(c) Dar Scout Media, Scout Chat Forum 2015

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni