Jumapili, 29 Machi 2015

SKAUTI WAPO KATIKA MAJONZI MAKUBWA

MHOMWA HATUNAYE TENA


Chama cha Skauti Tanzania kimepatwa na pigo kubwa baada ya kufariki aliyekuwa Kamishna Mkuu ndugu Lawrence Humphrey Mhomwa.

Enzi ya uhai wake Marehemu Lawrence Hamphrey Mhomwa (wa pili kutoka kushoto) akiwa na baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Baraza kuu wakifuatilia jambo kwa makini, ulifanyika tarehe 05 Januari 2013 katika ukumbi wa Don Bosco Upanga
Dar Es Salaam.

Kwa mujibu wa msemaji wa wana-familia ya marehemu Mhomwa alisema, "Mpendwa Lawrence alifariki tarehe 20.03.2015"

Marehemu Lawrence Mhomwa, mpaka anafariki alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC).

Marehemu ndugu Lawrence Hamphrey Mhomwa alizaliwa katika kijiji cha Ng'ombo Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma tarehe 18 Desemba 1958.

Marehemu Lawrence aliamia jijini Dar Es Salaam na kuishi na mjomba wake ndugu Gabriel Matao na kuanza Elimu ya Msingi katika Shule ya Uhuru Mchanganyiko mwaka 1967 hadi mwaka 1974 alipofaulu na kujiunga na Shule ya Sekondari ya Azania mwaka 1975 hadi 1978.

Skauti kikosi maalum cha pared wamebeba sanduku lenye mwili wa marehemu Lawrence Humphrey Mhomwa kuelekea kanisani kwa ibada.

Kamishna Mkuu wa Skauti Mhe. Abdulkarim Shah (Mb) alimuelezea marehemu Mhomwa alikuwa mtu shupavu na alikuwa kiongozi pamoja na mkufunzi wake katika nishani mbalimbali za Skauti alizopata Mhe. Shah, pia Kamishna Mkuu Mhe. Shah aliendelea kusema, " marehemu ndungu Lawrence Mhomwa alijiunga na Chama cha Skauti Tanzania mkoa wa Dar Es Salaam tangu alipokuwa katika shule ya Msing ya uhuru Mchanganyiko miaka ya 1970 na kuendelea na shughuli  za Skauti hadi alipoingia katika shule ya Sekondari ya Azania mwaka 1975.

Kamishna Mkuu Mhe. Shah (Mb) aliendelea kusema, " Akiwa shuleni Azania Marehemu Lawrence Mhomwa aliongeza juhusi na maarifa zaidi katika shughuli za Skauti na kutunikiwa nishani ya Kwanza ya Skauti (First Class) tarehe 03.09.1975, ambapo pia alichaguliwa kuwa kiongozi wa Kikosi (Patrol Leader), na baadae kuwa kiongozi wa kikundi (Troop Leader).

Skauti Mkuu Mhe. Mwantum Mahiza (Mkuu wa Mkoa wa Lindi) akisalimiana na Skauti alipowasili katika nyumba ya msiba wa Marehemu Lawrence Humphrey Mhomwa, tarehe 23.03.2015 Kinondoni Studio  jijini Dar Es Salaam.
Mhe. Shah (Mb) alizidi kufafanua kuhusu marehemu Lawrence Mhomwa kuwa, baada ya kumaliza Elimu yake ya Sekondari katika Shule ya Azania na huku akifanya kazi, Marehemu Lawrence Mhomwa aliendelea na shughuli za Skauti hadi kuteuliwa kuwa Kamishna wa Skauti Wilaya ya Kinondoni mwaka 1980 hadi 1985.

Marehemu Lawrence Mhomwa alishika nyadhifa mbali mbali.
Mwaka 1986 hadi 1990 alikuwa Kamishna wa Skauti Mkoa wa Dar Es Salaam, mwaka 1991 hadi 2001 aliteuliwa kuwa Kamishna Mkuu Msaidizi Mafunzo,. Makao Makuu ya Chama cha Skauti Tanzania.
Mwaka 2002 hadi 2005 aliteuliwa kuwa Kamishna Mkuu Msaidizi Programu za Vijana, makao makuu ya Chama cha Skauti Tanzania na mwaka 2008 hadi 2012 aliteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania ambapo baada ya hapo alimwachia Mhe. Abdulkarim Shah (Mbunge wa Mafia)

Viongozi mbalimbali walihudhuria mazishi ya Marehemu Lawrence Mhomwa, Kamishna Mkuu Mhe. Abdulkarim Shah (wa pili kutoka kulia) akifuatiwa na aliyekuwa Skauti Mkuu ndugu Kipingu (aliyevaa suti wa tatu toka kulia) na Kamishna Mkuu Msaidizi Mambo ya Nje, Uhusiano wa Kimataifa, Mawasiliano na Jota-Joti Skauta Fredirick Peter Nguma (wa pili kutika kushoto)

Marehemu ndugu Lawrence Mhomwa alipata mafunzo mbalimbali ya Skauti ndani na nje ya Nchi, mafunzo ya Ujasiri na Maarifa, ikiwa ni pamoja na kupanda Mlima wa Kilimanjaro akiwa Skauti mwenye umri mdogo.

Marehemu pia ameshiriki katika kambi mbali mbali za Skauti ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na Jamboree ya Dunia ya Skauti kutimiza miaka 100 iliyofanyika nchini Uingereza mwaka 2007.

Mwaka 1978 alipata Mafunzo ya Mkufunzi Msadizi (ALT) Chama cha Skauti Tanzania katika kambi kuu ya Bahati mkoani Morogoro.

Mwaka 1994 alipata Mafunzo ya Mkufunzi Mkuu (Leader Trainer) kutoka kambi ya Skauti Nyeri, Kenya.

Hadi alipofariki, marehemu Lawrence Humphrey Mhomwa alikuwa Mkufunzi wa Chama cha Skauti Tanzania.

Enzi ya uhai wake, Marehemu Lawrence Humphrey Mhomwa akiwa katika utendaji kazi wa Skauti ofisini kwake Chama cha Skauti Tanzania.

Msemaji wa familia ya marehemu alizungumzia kuhusu marehemu katka shughuli zake za kazi, msemaji huyo alisema, Marehemu ndugu Lawrence Humphrey Mhomwa baada ya kumaliza Elimu yake ya Sekondari aliajiliwa na Hotel ya Kunduchi Beach iliyopo jijini Dar Es Salaam na kufanyakazi kama Mhudumu na baadae kuhamishiwa Idara ya Utunzaji bidhaa (store keeper) mwaka 1978 mwishoni hadi mwanzoni mwaka 1980.

Tarehe 30 Julai 1980 aliajiliwa na Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) kama mhudumu wa ndani ya ndege (cabin crew). Mwaka 1986 kutokana na utendaji wake mahiri wa kazi, alipandishwa Cheo kutoka Muhudumu Mkuu (Senior crew hadi kuwa Senior Fight Pursers).

Marehemu Lawrence Mhomwa alifanyakazi katika Idara mbalimbali ndani ya Shirika la ndege la Tanzania, ikiwa ni pamoja na Idara ya Mizigo (Cargo Department) pamoja na Idara Uendeshaji (Operation Department) mwaka 1990.

Aliendelea kusema kuwa, "Marehemu Lawrence Mhomwa alipata mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya Usafiri wa ndege na usalama ndani ya ndege. Mafunzo hayo pamoja na mengine ambayo yalimwezesha marehemu ndugu Lawrence Mhomwa kupandishwa cheo na kuwa Mkufunzi Mkuu (Chief Instructor) kutoka chuo cha Wahudumu wa ndege cha Shirika la Ndege la Tanzania.

Skauti mbali mbali waliudhuria maziko ya Marehemu Lawrence Humphrey Mhomwa kama wanavyoonekana katika picha wakiwa katika eneo la makaburi ya Kinondoni.

Viongozi wa Skauti wakiwa katika eneo la makaburi ya Kinondoni, kwa ajili ya mazishi ya ndugu Lawrence Mhomwa tarehe 23 Machi 2015. Kamishna wa Mkoa wa Dar Es Salaam ndugu Abubakar mtitu (aliyeshika mwamvuli) na Kamishna wa Wilaya ya Ilala ndugu Crispin .W. Majiya (wa kwanza kushoto) 

Msemaji kwa niaba ya wafanyakazi wenzake wa Shirika la Ndege la Tanzania, alimuelezea marehemu Lawrence Mhomwa kuwa, "Alikuwa mtu mahili sana, na kutokana umahili wake na mafunzo thabiti aliyoyapata kutoka katika Chama cha Skauti Tanzania pamoja na Shirika la Ndege la Tanzania, tarehe 13 Februari 1988 wakati ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania aina ya Boeing 737 ilipotekwa ikiwa safarini kutoka Dar Es Salaam kwenda Kilimanjaro, marehemu ndugu Lawrence Mhomwa ambaye alikuwa ndani ya ndege hiyo kwa siku hiyo, alifanya kazi kubwa sana ya kuwatuliza abiria walikuwa wanataka kupambana na watekeji wa ndege hiyo".

Msemaji huyo aliendelea zaidi kusema, "Kutokana na ushupavu na ujasiri wake huo, tarehe 26 Aprili 1989 katika sherehe za Muungano alitunukiwa NISHANI YA JUU YA USHUPAVU, na Rais wa awamu ya pili Mheshimiwa ndugu Ali Hassan Mwinyi, katika viwanja vya Ikulu jijini Dar Es Salaam". 

Kwa maelezo mengine ambayo Dar Scout Media iliyapata kutoka kwa msemaji wa familia ya marehemu Lawrence Mhomwa kuwa, Marehemu Lawrence Mhomwa pia aliwai kuwa Katibu wa Chama cha Wafanyakazi (COTWU) tawi la Uwanja wa Ndege wa Dar Es Salaam mwaka 2005 hadi 2011 na baade kuendele kuwa mmoja wa Wajumbe wa Chama hicho.

Pia, wahudumu wa ndani ya ndege wa Shirika la Ndege la Tanzania, walimuelezea marehemu Lawrence kuwa alikuwa mtu wa watu na wa kuigwa hakika watamkosa wa kuweza kumlinganisha.

Hadi alipofariki tarehe 20 Machi 2015Marehemu Lawrence Humphrey Mhomwa alikuwa anashikiria wadhifa wa Mkufunzi Mkuu (Chief Instructor) katika Chuo cha Wahudumu wa Ndege wa Shirika la Ndege Tanzania.

TAARIFA ZA UGONJWA HADI KUFARIKI KWAKE

Matatizo ya kuugua kwa marehemu Lawrence Mhomwa yaliaanza kiasi cha wiki nne (4) zilizopita, akisumbuliwa na matatizo ya maumivu katka koo.

Marehemu alikuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Regency na TMJ zote za jijini Dar Es Salaam na alikuwa akiendelea vizuri tu hadi usiku wa tarehe 19 Machi 2015 hali yake ilipobadilika ghafla, na asubuhi ya tarehe 20 Machi 2015 marehemu aliomba familia yake impeleke kwa Mchungaji kwa ajili ya maombi, akiwa njiani kuelekea kwa Mchungaji, hali yake ilibadilika tena, na familia kuamua kumpeleka hospitali ya Mwananyamala ambapo alifariki siku hiyo mchana.

Marehemu atakumbukwa daima kwa umahiri wake na utendaji kazi wake. Taasisi hizi mbili za Chama cha Skauti Tanzania na Shirika la Ndege la Tanzania, ambapo muda wote wa maisha yake amekuwa akizitumikia.

Marehemu Lawrence Humphrey Mhomwa ameacha Mjane na watoto wanne (4).


PICHA MBALI MBALI KATIKA MAZISHI YA MAREHEMU LAWRENCE MHOMWA















MWENYEZI MUNGU AIWEKE ROHO YA MAREHEMU LAWRENCE HUMPHREY MHOMWA MAHALA PEMA PEPONI, AMIN.



  • Dar Scout Media
  • Scout Chat
  • +255-655-095559
  • Scout Breaking News
  • +255-755-095559

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni