Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza, akizungumza jambo baada ya kuhitimisha matembezi (Tarehe 18/02/2017)
RAIS mstaafu ambaye pia ni Mdhamini wa Skauti Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi, leo (tarehe 18/02/2017) ameongoza matembezi ya hisani (Charity Walk) kwa ajili ya kuchangisha fedha za kufanikisha shughuli za Chama cha Skauti Tanzania kutoka kwa wadau na marafiki wa skauti kuelekea maadhimisho ya siku ya Skauti Afrika yanayotarajiwa kufanyika Machi 8 hadi 11 na Miaka 100 ya Skauti Tanzania (1917 - 2017) matukio yote mawili yanategemea kufanyika mwaka huu jijini Arusha.
|
Matembezi hayo ya hisani yameanzia katika kiwanja cha Skauti kilichopo Upanga jijini Dar es Salaam na kuishia katika bwalo la Maofisa wa Polisi (Police officers Mess) la Oysterbay kuanzia saa 12 asubuhi na kufikia tamati majira ya saa nne asubuhi.
Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi (wa pili kushoto) alipofika katika viwanja vya Bwalo la Polisi, Oyster Bay jijini Dar, wakati alipohitimisha matembezi ya hisani. Kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako aliyeungana naye. |
Aidha, Rais Mstaafu ALI HASSAN MWINYI, amezindua mfuko wa kuchangia maandalizi ya mkutano wa Skauti wa Afrika, uanaotarajiwa kufanyika Arusha, Machi mwaka huu ambapo ameonyesha kufadhaishwa na baadhi ya wazazi wanaoshindwa kuwalea watoto wao katika roho na kweli hivyo kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa maadili na kihalifu ikiwemo matumizi ya vileo na dawa za kulevya.
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa zaidi ya watu 5,000 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya bara hilo wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano wa mwaka wa maskauti kuanzia Mach 8 mpaka 11 mwaka huu Mkoani Arusha, ikiwa ni maadhimisho ya kila mwaka ya siku ya skauti Afrika yanayokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 1OO ya skauti Tanzania.
Mzee Mwinyi, ambaye ni Mwenyekiti wa baraza la wadhamini wa skauti Tanzania,mwenye umri wa miaka 93 sasa, akiwa bado ni mkakamavu na mwenye siha njema, alitembea kilometa 6.5 kutoka Makao makuu ya skauti Upanga mpaka viwanja vya bwalo la maafisa Polisi Ostabei, katika matembezi ya hisani kuchangia maandalizi ya mkutano huo unaotarajiwa kugharimu shilingi milioni 800.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na mafunzo ya Ufundi, Profesa JOYCE NDALICHAKO, ambaye kwa mujibu wa katiba ya skauti ni Rais wa skauti kutokana na madaraka yake, amewasihi wazazi kuwapeleka watoto wao skauti wakajifunze maarifa, stadi za maisha na uzalendo, badala ya kuwaacha kama mifugo isiyo na mchungaji na katika hatua nyingine, amewaonya walimu wote amabo shule zao zitabainika kuwa vijiwe vya wanafunzi kujifunzia mambo yasiyofaa, serikali haitawavumilia.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa matembezi hayo, Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza, alisema kuwa chama hicho kinatarajiwa kusherehekea Siku ya Skauti Afrika na kuadhimisha miaka 100 tangu Skauti kuingia Tanzania Bara (Tanganyika). Chama hicho hapa nchini kilianza mwaka 1917 na mwaka huu wa 2017 kinatimiza miaka 100.
Uchangishaji mwingine wa fedha kwa njia ya chakula (Dinner Gala Fund Raising) unategemea kufanyika Februari 24 katika Hoteli ya Serena ya ijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake kamishna Mkuu wa Skauti Abdulkarimu Shah amesema bado wanaendelea kuwahamasisha vijana kujiunga katika chama hicho ili kuwa waadilifu, wajasiri, wabunifu na wenye maarifa ili kufanikiwa na kuepukana na magonjwa yanayoepukika ikiwemo Ukimwi.
Maadhimisho hayo yatafanyika juni 24 hadi julai mosi mwaka huu mjini Arusha, yenye kauli mbiu inayosema “kuwajenga wazalendo na kufanya kazi kwa bidii kwa maendeleo ya nchi”.